TAMBUA/ELEWA UMUHIMU WA MALAIKA WA VITA WANAVYOWEZA KUTUSAIDIA KUPIGANA VITA VYA KIROHO.
1.VITA VYA KIROHO.
Ni vita inayofanyika katika ulimwengu wa roho.Ulimwengu wa roho ni mahali ambapo roho zinaishi ( habitat of spirits), huu ulimwengu wa roho umegawanyika sehemu kubwa mbili:-
1.Ulimwengu wa roho katika nuru
2.Ulimwengu wa roho katika giza
1.Ulimwengu wa roho katika nuru
Ni ulimwengu ambao Mungu Mtakatifu na malaika( ikijumuisha wenye uhai 4 na wazee 24) wanaishi.Mtu yoyote aliyeokoka anauwezo wa kuishi hili eneo kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ili uweze kulifahamu vizuri hili eneo unamuhitaji Roho Mtakatifu maana yeye ndiye mwenyeji wa hili eneo.
"Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu" (WAEFESO 2:6)
Kwahiyo kumbe yoyote aliyeokoka anaweza akaishi katika ulimwengu wa roho katika nuru hata akiwa bado yuko duniani anaishi!
2.Ulimwengu wa roho katika giza
Ni eneo ambalo Shetani, majini, mapepo, mizimu na kila aina za roho chafu zinaishi.Mtu yoyote aliyeokoka amepewa mamlaka ya kulitawala hili eneo kuanzia Shetani na majeshi yake yote.
"Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru" (LUKA 10:19)
Kumbe kwasababu tumeketishwa na Kristo katika ulimwengu wa roho tumewekwa juu ya ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo ( WAEFESO 1:20-23).
Njia ya maombi pekee ndiyo ambayo inaweza kumsaidia mwamini aliyeokoka kupigana vita vya kiroho.Maombi yoyote kwa asili ni vita haijalishi hayo maombi unayoomba mbele za Mungu unaomba kwa kupekeka hoja mbele za Mungu au kwa njia ya mahojiano, unaweza ukafanya maombi kwa njia ya mahojiano na Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Lakini wakati wa kupokea majibu ya maombi uliyoyaomba ni vita! Jiulize haya maswali wewe mwenyewe kwani ni maombi mangapi uliomba kwa Mungu akakuhaidi kabisa atakupa lakini mpaka sasa hauoni majibu ya maombi uliyoomba? Unafikiri ni kwanini? Si unaona sasa ulizungumza na Mungu kwa njia ya mazungumzo njia ya amani kabisa lakini angalia sasa kwenye eneo la kupokea majibu yako.Utagundua sasa kumbe kati ya mapmbi kumi uliyoomba umejibiwa moja. Katika siri ambayo watoto wa Mungu wengi hawaifahamu katika maombi ni hii kutojua kwamba Shetani anapigana sana vita na eneo la kupokea majibu ya maombi wanayoomba!
Kuna hatua 2 za maombi ambazo huwa zinapitia mpaka kufikia hatua ya kujibiwa maombi uliyoomba:-
1.Wakati unaomba maombi yako kwenda mbele za Mungu.
2.Wakati unasubiri majibu ya maombi uliyoomba kutoka kwa Mungu.
-Waombaji wengi wamefaulu hatua ya kwanza ya kupeleka hoja zao mbele za Mungu. Japokuwa maombi haya bado ni vita pamoja na kwamba unampelekea Mungu maombi au hoja zako. Utanielewa nina maana gani.Lakini waombaji wengi wamefeli kwa kiasi kikubwa katika hatua ya pili ya kupokea majibu ya maombi waliyoomba mbele za Mungu. Wengi wakimwomba Mungu maombi yao Mungu akasema atawapa wanaridhika, wanaacha kuomba wanarelax (wanajiachia ) wakifikiri Mungu ndiye atawashughulikia upatikanaji wa maombi wanayoyaomba mpaka yaonekane katika macho ya damu na nyama. Hee hee kumbuka kanuni ya kiroho jinsi ilivyo pamoja na kwamba Mungu atakupa ruhusa ya kukupa ulichohitaji ila mwenye kazi ya kuumba ulichokihitaji ni wewe ili kiweze kutokea kwa macho ya damu na nyama.
Hii imesababisha waombaji wengi kukata tamaa kwasababu wanafikiri Mungu ni mwongo! Wengine wanafikiri ni majaribu Mungu anawapitisha lakini kumbe sivyoo. Mungu hapendi watu wake waishi kwa shida wala majuto Mungu anawapenda watu wake anataka waishi kwas furaha na amani. Na Mungu huwa anaachilia jaribu kwa kusudi maalumu. Kwahiyo utakubaliana na mimi kwamba jaribu ni " special case" kwasababu maandiko yanasema Mungu anatuwazia mema kila iitwapo leo maana yake hata kabla hujaomba kusudi la Mungu ni kukuona unafanikiwa kwenye maisha yako.
Natamani upate hasira ndani yako kuanzia sasa kwamba mwenye shida ya kutojibiwa maombi yako ni wewe mwenyewe. Wewe ukisimama sawa sawa nilazima ulichoomba mbele za Mungu ukipate madamu tuu yeye Mungu ameruhusu upate ulichoomba. Shetani anafahamu kabisa Mungu huwa anaachilia majibu kwenye ulimwengu wa roho ili watoto wake wakipate. Shetani kazi yake huwa anahakikisha anapigana kwenye ulimwengu wa roho ili usipate ulichoomba kwasababu amejaa hila! Maandiko yanasema ivi:-
"Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka" (MATHAYO 11:12)
Unaona sasa! Unaelewa nini maana ya ufalme wa mbinguni?
Tusome MATHAYO 5:9- 10 angalia inavyosema:-
"Basi ninyi salini hivi, Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni"
Umeona sasa ufalme wa mbinguni kuja haimaanishi Mungu ashuke pamoja na malaika zake hapa duniani hapana! Mungu anautaratibu katika utawala Mungu ni Roho (YOHANA 4:24) hawezi kuja duniani kutawala bila kutumia mwili( mtu/mwanadamu) ni lazima amtumie mwanadamu ili aweze kutawala hiyo ni kanuni aliyojiwekea. Mungu anakanuni zake kanuni aliyoiweka yeye mwenyewe huwa haitengui hata siku moja hiyo ni kanuni aliyoiweka mwenyewe nilazima aifuate. Unaweza kujiuliza maswali kwanini Mungu hakuamua kumtuma Yesu aje kama nguvu fulani ivi haionekani kwa macho ikawa ni sauti tuu iseme mimi ni mwana wa Mungu nimeagizwa kuwaokoa wanadamu. Lakini unafikiri Mungu angeamua kufanya hivyo angeshindwa? Kwahiyo Mungu anaweza kufanya chochote lakini anaheshimu sana kanuni na taratibu alizojiwekea yeye mwenyewe.
Kwahiyo sasa kumbe Mungu anamtumia mtu kuushusha ufalme wake hapa duniani. Lakini kuuteka huo ufalme uje duniani mwenye nguvu peke yake ndiye anayeweza kuuteka! Sasa ufalme wa Mungu umebeba mambo mengi sana ndani yake lakini elewa tuu ufalme wa Mungu umebeba kila kitu chenye kumfanikisha mwanadamu! Maombi ya aina yoyote unatoyaomba yamebebwa ndani ya ufalme wa Mungu! anayetakiwa kuushusha huo ufalme ni wewe.
2.MALAIKA
Ni viumbe ambao wanamfano wa mwili wa wanadamu (Mwanzo 32:24-30, Ebrania 13:2), wanaweza kugusika ni viumbe ambao wanaushirika wa karibu sana na Mungu. Malaika wa vita kazi yao kubwa ni kumsaidia mwanadamu kupigana vita vya kiroho.Kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaleta majibu ya maombi uliyoomba kutoka kwa Mungu.
"Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazunguka wamchao na kuwaokoa" (ZABURI 34:7)
Kwahiyo katika ulimwengu wa roho, wako malaika ambao wanamsaidia mwanadamu kupigana vita vya kiroho wale wamchao! Watu wengi sana wanaamini uwepo wa Roho Mtakatifu hawaamini uwepo wa malaika wanaowasaidia kupigana vita vya kiroho.Kumbuka Roho Mtakatifu anatusaidia kuomba maombi tuliyonayo (Rum 8:26) lakini kwenye eneo la kuyaumba majibu ya maombi uliyopokea kutoka kwa Mungu muhusika ni wewe. Ndio maana maandiko yanasema ninyi ni miungu. Yaani kwa mfano unapoingia kumwomba Mungu akupe gari, unahitaji msaada wa Roho Mtakatifu ili akusaidie kuomba mbele za Mungu. Roho Mtakatifu anakuja na majibu kutoka kwa Mungu kwamba Mungu atakupa either siku fulani au mwezi fulani au mwaka fulani. Hapo umepokea majibu ya maombi lakini mwenye kazi ya kusimamia hilo gari uliloomba mpaka litokee katika macho ya damu na nyama ni wewe mwenyewe.
DANIELI 10:11-15 inasema ivi:-
"Akamwambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima, maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli, kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekesha mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja kwaajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja, bali tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia, nami nikamwacha huko paoja na wafalme wa Uajemi".
Sasa umeona kumbe Danieli alijibiwa maombi yake tangu siku ya kwanza lakini majibu ya maombi yaliyokuwa yamebebwa na malaika yalipingwa na ufalme wa Uajemi siku ishirini na moja kwasababu malaika alikuwa hana nguvu ya kupigana na huo ufalme. Kilicho msaidia huyo malaika ni malaika Mikaeli ndio akapata upenyo wa kutoroka kumpelekea Danieli majibu ya maombi aliyoyaomba. Lakini kumbuka Danieli alikaa siku ishirini na moja kwenye maombi. Swali la kujiuliza mwenye makosa ni nani? Je ni Mungu ambaye alitoa majibu kwa wakati tangu siku ya kwanza ya maombi ya Danieli? Je ni malaika ambaye alikuwa ni mdhaifu kupigana vita juu ya ufalme wa Uajemi? Au ni Danieli ambaye hakuwa na ufahamu wa kutambua katika ulimwengu wa roho kuna hila za Shetani?
Majibu tunayapata moja kwa moja kuwa Danieli kilichosababisha acheleweshewe majibu ya maombi yake ni kwamba hakuwa na ufahamu juu ya maombi ya vita. Kwasababu alikuwa na mamlaka kabisa ya kuamuru ufalme wa Uajemi upigwe ili maombi yake yajibiwe kwa wakati.Kwahiyo kumbe Danieli angefanya maombi ya vita angepokea majibu ya maombi yake siku ile ya kwanza alipoingia kuomba.
Mambo muhimu ya kufahamu juu ya malaika wa vita
1.Malaika wa vita wanabeba wasifu wa mwombaji.
2.Wanasikiliza amri ya mwombaji.
3.Utendaji kazi wao unategemeana sana na mazingira ya kiroho ya mwombaji.
Wasifu wa malaika wa vita anavyotakiwa kuwa katika ulimwengu wa roho
1.Anatakiwa awe na vazi la kisasi
2.Anatakiwa awe amejifunga kweli kiunoni
3.Anatakiwa awe amejifunfa deraya/dirii kifuani
4.Anatakiwa avae utayari miguuni
5.Anatakiwa awe ameshika ngao mkono wake wa kushoto
6.Anatakiwa awe na upanga wa roho ameushika mkono wake wa kulia
7.Anatakiwa awe na chepeo ameivaa kichwani
WAEFESO 6:10- 17 inasema ivi:-
"Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama, bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi wa pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwasababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa injili ya amani, zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chepeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu."
Paulo alijua kwenye ulimwengu wa roho kuna hila za Shetani na iko vita ndio maana aliwaambia Waefeso twaeni silaha zote za Mungu! Kwasababu alijua wako malaika ambao wanatakiwa wabebe huo wasifu wa hizo silaha za vita ili waweze kushinda vita kwenye ulimwengu wa roho! Sasa inapoingia kwenye maombi ya vita nilazima uvae silaha zote za vita. Ili malaika wako wanaokusaidia kupigana vita vya kiroho wasipigwe, washinde vita. Kwasababu hao malaika watachukua wasifu wako, silaha ulizovaa ndio watakazo zivaa, kama utaingia kwenye hayo maombi ukawa umeshika upanga tuu peke yake ujue utakuwa na uwezo wa kuua lakini mishale ya moto ya adui ikija utashindwa kuizuia kwasababu hauna ngao.Kwahiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuvaa silaha zote za vita ili uweze kupigana vita vizuri vya kiroho na kushinda ili majibu yako yaje kwa wakati!
MBO YA KUZINGATIA UNAPONINGIA KUPIGANA VITA VYA KIROHO
1.Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita uwe na WIVU ambalo ndio VAZI LA KISASI linalovaliwa mwili mzima.
KISASI
Ni hali ya kuchukia kuonewa na Shetani juu ya jambo ambalo amelifunga kwenye ulimwengu wa roho.Inawezekana ikawa ni kufeli kwenye masomo Shetani amefunga, inawezekana ikawa ni roho mbaya za kurithi Shetani amefunga kwenye ulimwengu wa roho. Ili ushinde vita unatakiwa kuichukia hali mbaya uliyonayo ya kutofanikiwa hiyo itakupa nguvu ya kufanikiwa katika vita unayoiendea.(YAKOBO 4:7)
"Akajivika haki kama deraya kifuani, na chepeo cha wokovu kichwani pake, akajivika mavazi ya kisasi yawe mavazi yake, naye alivikwa wivu kama joho" (ISAYA 59:17).
2.Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita unakuwa na NIA ya kupigana hiyo vita ambayo ndiyo KWELI inayovaliwa kiunoni.
NIA
Ni kiu ya kutaka kuona kuona kitu kinaenda kufanyika katika ulimwengu wa roho.Kwahiyo muombaji yoyote anapoingia kwenye vita vya kiroho nilazima awe na nia, haitakiwi unapoingia kwenye vita vya kiroho kukata tamaa. Inaweza ikawa unaingia kwenye maombi ya kuvunja madhabahu za miungu kwenye ukoo wako inatakiwa uwe na nia mpaka uone hizo madhabahu zinazokufuatilia za ukoo wako zinavunjika.
" Kwahiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi, mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wa Yesu Kristo" (1PETRO 1:13)
Kwahiyo unatakiwa kuwa na nia unapoenda kupigana vita nia ndiyo iliyomsaidia Yesu kulitimiza kusudi la Mungu alipokuwa duniani!
"Iweni na nia hiyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo ndani ya Kristo Yesu" (WAFILIPI 2:5).
3.Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita unakuwa na haki ambayo ni DIRII/DERAYA YA HAKI inayo valiwa kifuani.
HAKI
Ni uhalali wa kupokea kitu ambacho unastahili kukipokea. Mtu mwenye dhambi haruhusiwi kupigana vita vya kiroho! Haki inapatikana kwa njia ya toba, Hakikisha hauingii kwenye maombi ya vita kama haujaomba rehema .
"Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana akiomba kwa bidii" (YAKOBO 5:16b). Haki inapatikana kwa kuomba rehema hakikisha hauingii kwenye maombi ya vita ukiwa haujaomba rehema.
4.Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita uwe na AMANI ambayo ndio UTAYARI unavaliwa miguuni.(ISAYA 52:7)
"Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao."(WAEBRANIA 12:14)
Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita uwe na amani na watu wote usiingie kwenye maombi ya vita huku ukiwa unavinyongo na watu, usiingie kwenye maombi ya vita ukiwa umewabeba watu moyoni, usiingie kwenye maombi ya vita ukiwa na uchungu moyoni waachilie hao watu moyoni mwako na uwasamehe ndipo uingie kwenye maombi ya vita.
5.Hakikisha unaloingia kwenye maombi ya vita uwe na IMANI ambayo ndio ngao inashikwa mkono wa kushoto.
"zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yenye moto ya yule mwovu" (WAEFESO 6:16)
"Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu, na huku ndiko kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu."(1YOHANA 5:4)
Hakikisha unaingia kwenye maombi ya vita ukiwa na imani usiingie kwenye maombi ya vita wakati hauamini hiyo vita utashinda.
6.Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita uwe UMEOKOA ambayo hiyo ni CHEPEO inavaliwa kichwani.(ISAYA 59:17)
"Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani, na upendo, na chepeo yetu iwe tumaini la wokovu" (1THESALONIKE 5:8)
Kwahiyo usiingie kwenye maombi ya vita ukiwa haujaokoka.Yaani hujamkiri Yesu kuwa ni Bwana na kuamini Mungu alimfufua katika wafu (WARUMI 10:9)
Kwahiyo kama hujaokoka hauruhusiwi kupigana vita vya kiroho aliyeokoka peke yake ndiye mwenye haki ya kupigana vita vya kiroho!
7.Hakikisha unapoingia kwenye maombi ya vita unakuwa na NENO LA MUNGU ambalo ndio UPANGA WA ROHO unashikwa mkono wa kulia.
"Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali, katika kivuli cha mkono wake amenisitiri, naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa, katika podo lake amenificha, (ISAYA 49:2)
"Kwasababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii, nimewaua kwa maneno ya kinywa changu, na hukumu yangu ikatokea kama mwangaza" (HOSEA 6:5)
Kwahiyo unapoingia kupigana viga vya kiroho hakikisha unakuwa na neno la Mungu kwasababu maandiko yanasema neno la Mungu huwagawa nafsi na roho na mafuta. Ni hakika unapotumia NENO la Mungu kwenye maombi ya vita Mungu anafanya! Kwa mfano ni wachawi ndio wametawala kwenye ukoo wako/ mji wako unaweza kuingia kwenye maombi kwa kutumia neno la Mungu linalosema "Usimwache meanamke mchawi aishi" jifunze kutumia neno unapoingia kwenye maombi ya vita. Usiingie kwenye maombi ya vita kama hauna neno la Mungu.
Ili maombi yako yajibiwe kwa wakati nilazima uzingatie haya mambo 7 unapoingia kwenye maombi ya vita.Kwasababu malaika wa vita huwa wanabeba wasifu/ mfano wa mtu anayeingia kupigana hiyo vita kwahiyo kama ikitokea haujavaa viatu ambao ni Utayari malaika naye hatavaa, usipovaa chepeo malaika naye hatavaa, usipokuwa na upanga naye malaika hatashika, kadhalika na silaha nyingine zote.Angalia sasa kama malaika akiwa kwenye ulimwengu wa roho hana silaha zote za vita.Kwanza anakuwa dhaifu, na anapokosa nguvu anashindwa kurejesha majibu ya maombi uliyoomba.
Zaidi sana kinachotokea malakia wa vita akikosa nguvu ya kupigana na falme za giza kwenye ulimwengu wa roho, unaweza ukapata majibu ya maombi yako kwa kuchelewa sana kama ilivyotokea kwa Danieli. Au usipate majibu ya maombi yako kwa kunyang'anywa majibu ya maombi yako ambayo umeomba. Huenda uliyaangaikia kwa kufunga na kufanya maombi ya mda mrefu. Hapo ndipo huwa unafika wakati waokovu wengi wanakata tamaa nakufikiri Mungu amewaacha, na Mungu anasikitika anawahurumia kwasababu wamekosa kuwa na maarifa! (ISAYA 5:13)
Ngoja nikupe siri hii hakuna kilichochema kinachotoka kwa Ibilisi kila kilichochema kinatoka kwa Mungu!
"Kila kutoa kuliko kwema , na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga, kwake hakuna kibadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka" (YAKOBO 1:17)
Shetani amejaa hila lengo lake kubwa ni kuhakikisha ulichomwomba Mungu hakitokei katika macho ya damu na nyama kwenye maisha yako. Kwahiyo sasa unapoingia kwenye maombi na hauna silaha za vita, malaika wa vita anakuwa dhaifu, kinachotokea ananyang'anywa majibu ya maombi yako na malaika wa kipepo halafu yanahifadhiwa katika ulimwengu wa giza! Unajua ni kwanini watu wakiendwa kwa waganga wakienyeji kuomba mali, fedha, utajiri, magari, kuwa na akili darasani, kuwa na upako na miujiza wanapata? Kwasababu kila kilichochema kinatoka kwa Baba wa mianga ambaye ni Mungu lakini kwanini wapate kutoka kwenye ufalme mwingine? Sababu kubwa ni kwamba waombaji wengi huwa wanafikiri kupokea majibu ya maombi yao ni simple kumbe sio rahisi kama wanavyofikiri wanaingia kwenye maombi hawana silaha za vita. Mungu ni kweli anawasikia na anawajibu shida inakuja kwenye kupokea majibu ya maombi yao. Kwahiyo falme za giza zikipata nguvu ya kuwashinda malaika wanaokusaidia kupigana vita rohoni kwasababu ya kukosa nguvu. Hizo falme zinaiba majibu ya maombi yao na kuyahifadhi kwenye ufalme wao.Ndio maana mtu akienda kwenye ufalme wao kuomba chochote anapata kumbe ni majibu ya maombi ya watoto wa Mungu yaliibiwa na ufalme wa giza kwa hila. Wengine waliomba wapate watoto, wengine kufanikiwa kwa kila namna na Mungu aliwaahidi kabisa anawapa lakini mpaka leo hii hawajapata! Shida ni nini tatizo ni hila za Shetani na amekushinda kwasababu hukutumia kanuni za kiroho ulipoenda kupigana vita.
Ni kiu yangu sasa hasira iumbike ndani yako juu ya Shetani ili uweze kupigana vita vya kiroho.Kwasababu kama umeokoka ni haki yako kufanikiwa! Yaani kufanikiwa kwa aliyeokoka ni haki yake. Unachotakiwa kukifanya sasa fuata kanuni za kiroho unapoingia kwenye maombi yako ya vita halafu hata kama Mungu amekuahidi kukupa kitu kwenye maisha yako usiache kuomba. Endelea kusukuma kwa maombi hicho ulichoomba mpaka kitokeee katika macho ya damu na nyama.
Mungu wabinguni akubariki sana ninaamini kuna eneo umevuka.Mungu akusaidie by
Apostle BARAKA SHIBANDA under Godlypowermanifestationministry.
No comments:
Post a Comment